Tuesday, 24 September 2013

Kichwa chako kinakukwamisha kwa yafuatayo !!


Moja kati ya vitu vigumu maishani, ni kuishi kama unavyotaka wewe maisha yawe.
Mara kwa mara utajikuta unachanganywa na vitegemezi kama chakula, manunuzi, matukio ya televisheni, mitandao ya kijamii na hata simu za mkononi.
Vitegemezi hivi vinachangia kukuondoa katika uhalisia wako wa maisha na kukusahaulisha hisia za kweli na unajikuta unapoteza fursa zilizopo.
Unapokuwa mpweke ndio unapata muda wa kuzitafakari hisia zako halisi kwa kina:
uoga, hofu, furaha, hasira, au hata huzuni.
Haijalishi hisia zako ni hasi au chanya lakini zinakupa picha halisi ya unataka nini katika maisha.

Tuangalie kwa pamoja sababu zinazochangia 
mpaka unapoteza fursa zilizopo:

1.KUTAKA KUFANYA KILA KITU:

Karibu kila binadamu kuna kipindi anahisi anapitwa na vitu vinavyofanyika duniani, ambavyo anatamani pia angekuwa anavifanya.
Lakini hakika unaweza ukazunguka kila sehemu na kutaka kujihusisha na kila kitu, mathalani  kufanya kazi,au burudani masaa 24  bila kulala lakini bado hautaweza kujihusisha na kila kitu.
Kwahiyo achana na hisia za kwamba unapitwa na mambo na tambua kila unachotakiwa kufanya kipo katika mazingira yako.

2.KUKWEPA MAUMIVU NA KUSHINDWA:

Usijaribu kuukimbia ukweli wa maisha yanayokukabili, kwani maumivu na kushindwa ndio vitu vinavyosaidia ukuaji wako wa akili.
Kumbuka, kuna tofauti kati ya kuwa katika mazingira ya kushindwa na kuwa umeshindwa tayari .
Hautaweza kuvikimbia vitu hivi mpaka viwe vimekufundisha unachopaswa kukijua katika maisha yako, ili uchukue hatua nyingine mbele.

3.KUENDELEA KUSHIKILIA KUMBUKUMBU ZA ZAMANI:

Usijaribu kutumia muda wako mwingi kufikiria mambo mabaya ambayo yalishapita kwani kufanya hivyo ni kuyaruhusu yaharibu wakati uliopo.
Usijaribu kuishi wakati mwengine, unatakiwa ukubali kumaliza hizo kumbukumbu ili uanze kujenga mwanzo mpya.
Anza kufunga kumbukumbu za mambo mabaya ya zamani sasa na jua hayatakuongoza unapotaka kufika.

4.KUJIKUMBUSHIA MATUKIO YA KUSHINDWA:

Kama ukiendelea kujisimulia historia za matukio uliyoshindwa kichwani mwako, utayaamini na kujiona ni mtu wa kushindwa daima.
Swali ni: Historia unayojisimulia inakutia nguvu?
Usiendelee kuweka makosa yako kichwani, kwani uzito wake utaangusha uwezo wako halisi.
Unapaswa utambue kuwa kila kitu mwanzo huwa ni kigumu kabla hakijawa rahisi.

5.KUIGIZA MAISHA YA MWENGINE:

Vita kali zaidi uliyowahi kupigana nayo ni vita ya kutaka kuwa wewe, hivyo ulivyo sasa.
Hautawezi kuwa wewe kama kila siku unajitafuta kwa watu wengine.
Kumbuka, unapoigiza maisha ya mtu mwengine unapoteza nafasi ya kujitumia wewe mwenyewe na uwezo wako wa asili utakufa kwa kuwa hautumiki.

6.PICHA YAKO KICHWANI YA UNAVYOTAKA VITU VIWE:

Moja kati ya vitu vinavyokuangusha katika maisha ni picha unayoijenga kichwani 
na kutaka kila kitu kiwe kama ulivyokiona wewe mawazoni.
Maisha yanasonga na mara kwa mara sio kama ulivyotaka yawe, bali kadri yalivyopaswa yawe.
Maisha ni kama muziki unaochezwa ambao haukuuchagua, lakini unaweza ukachagua namna ya kuucheza.

7.KUJIONA UNA KASORO:

Usijihukumu mwenyewe, kuna watu wengi wanatamani kufanya hiyo kazi kwa ajili yako.
Fanya unayopaswa kufanya kwa uwezo wako na mengine yanayobaki yasalimishe kwa wengine.
Jipende na jionee fahari na kila kitu unachofanya hata kama umekosea kwani hata makosa yanaonyesha ulijaribu kufanya.

8.KUENDELEA KUSUBIRI:

Acha kuendelea kuisubiri kesho, kwani muda wa leo hautaupata tena.
Maisha ni mafupi sana kama kila siku unaomba udhuru.
Achana na mitazamo ya kutaka kufanya kila kitu kesho, anza leo kufanya hatua japo moja ya jambo lako kwa ujasiri.
Kama huna hakika ni njia gani hasa unayopaswa kupita, kufuata moyo wako ndio njia bora iliyobaki.
KAA TAFAKARI NI JAMBO LIPI KATI HAYO HAPO JUU LIMEKUWA TATIZO KWA WEWE KUFIKIA MALENGO YAKO.

ANZA KULISHUGHULIKIA SASA NA UTAONA MATUNDA YAKE

Monday, 16 September 2013

Je? unapingwa katika jambo lako??,Fuata haya utafanikiwa !!


Katika maisha yetu tunayoishi hakuna mtu hata mmoja, ambaye hana watu wanaompinga hata kama anafanya jambo jema.
Na wengi wanapokutana na fitina za watu hao hujiona hawafai na wanataka kukata tamaa kwa kile wanachofanya katika maisha.
Mara nyingi wamekuwa wanaumizwa na maneno yanayosemwa na watu hao kuwahusu wao.

Hebu tuangalie kitu gani ufanye pindi unapokabiliwa na mazingira kama hayo:

1.USIACHE KUJIPENDA:

Mahusiano yako na nafsi yako yanatakiwa uyaangalie kwa ukaribu sana kwa kujitunza,
kwani ndio msingi ambao maadui wanajitahidi kuubomoa kwanza.
Wakishafanikiwa kukufanya ukajichukia basi kazi ya kukuharibu 
inakuwa ni rahisi mno.
Hakuna mtu ambaye anajichukia yeye halafu akafanikiwa kuwa na mahusiano mazuri na wengine.

2.FANYA KILE NAFSI YAKO INAKWAMBIA NI SAHIHI:

Usiogope kutembea barabara ya peke yako, na usiogope kuelekeza nguvu zako huko kwasababu tu ya maneno ya watu wengine.
Usiruhusu ujinga, maigizo ya watu na fikra zao hasi zikufanye usifikie ndoto zako.
Endelea kufanya kile kitu moyo wako unakwambia ni sahihi na unafurahia.
Hii ni kwasababu pale wewe unapofanya kitu sahihi ambacho nafsi yako inapenda hakuna atakayeweza kukuangusha kirahisi. 

3.FUATA NJIA ZAKO:

Kila siku hapa duniani inatoa nafasi kwa kila binadamu kufanya mabadiliko katika maisha yake.
Jitahidi kuitumia kufanya mabadiliko unayoyatamani usiruhusu mtu mwengine akubebeshe mzigo usiouhitaji.
Fanya hayo ukijua wazi kuwa pamoja na kwamba kuna watu wanachukia, lakini pia kuna wengine wanapenda unachofanya.

4.FANYIA KAZI MALENGO YAKO:

Unatakiwa ufanyie kazi malengo yako makubwa na ambayo unaona yanatekelezeka hata kama kuna watu wanakwambia hayawezekani.
Tambua kuwa mafanikio yanakuja kwa kufanyia kazi malengo yako.
Ile shughuli ambayo unaipa muda mwingi kila siku ndiyo inayoamua wewe uwe nani, kwahiyo tumia muda mwingi katika kutimiza malengo yako.

5.BADILISHA LENGO PALE UNAPOONA MAZINGIRA YAMEBADILIKA:

Kuna kipindi unaweza ukapanga lengo la kufanya shughuli fulani kutokana na mazingira kufungua fursa na umeiona.
Lakini baada ya muda mazingira hayo yakabadilika, usiwe mgumu kutafuta lengo mbadala hata kama la mwanzo ulitumia muda mrefu kuliandaa japo kuna watu watakushauri usibadilike.
Maisha siku zote hayatabiriki, lakini yanafungua milango kwa watu kutimiza ndoto zao.

6.USIWE MTU WA VISASI:

Tumia muda wako mwingi kufanya mambo yako ya muhimu kuliko kukaa na kufikiria namna ya kumlipizia 
kisasi mtu aliyekukosea.
Wengi watakushawishi ufanye hivyo ili upoteze dira na mipango yako kwa kushughulika na maisha ya watu na kuacha kufanya mambo yako.
7.ONYESHA UKARIMU NA UPENDO KWA WATU:

Usiwe mtu unayechagua watu wa aina fulani, ndio wa kuwaonyesha upendo kwa kuwa wanamchango kwako.
Japo hata ukifanya mambo mema vipi bado kuna watu watakushauri uache.
Jitahidi kuwafanyia matendo ya upendo na ukarimu watu unaokutana nao, kwani ukweli ni kuwa vile unavyowatendea wao ndivyo na wewe utakavyotendewa.

8.TETEA WATU WANAO ONEWA:

Mara nyingi unakutana na watu usiowafahamu au unaowafahamu, wakiwa katika matatizo ya kunyanyaswa. 
Usiache kuwatetea pale unapoona una uwezo wa kutoa msaada na ukawatoa 
katika hilo tatizo.
Ukifanikiwa kufanya tendo kama hilo ndani yako unajengeka moyo wa kishujaa wa kujiona una mchango katika jamii yako 
na watu watakujali.


YAWEZEKANA KABISA UKAWA KATIKA ENEO AMBALO WATU WENGI WANAOKUZUNGUKA HAWAKUPI USHIRIKIANO WA VITU UNAVYOTAKA KUFANYA.

KWA KUPITIA MAMBO HAYO HAPO JUU UNAWEZA UKAWEZA KUPAMBANA NAYO NA MWISHO WA SIKU UKAWA MSHINDI.

Friday, 13 September 2013

UMEKATA TAMAA??.Ukimaliza kusoma hapa hutabaki ulivyo.


Si kila mwenye mafaniko leo hii,
 aliyapata kwa mara ya kwanza
 alipojaribu.
Mara nyingi ni watu ambao walijaribu mara nyingi bila mafanikio,
 kabla hawajapatia na 
kufanikiwa.

Na wengi wao ni wale,
 waliokuwa wamejitolea kupambana 
na vikwazo 
kutoka kwa watu
 mbali mbali na mifumo.

Wanapovuka hatua hii ya vikwazo,
 wengi wao 
wanakosa majibu ya moja kwa moja wamefikaje hatua hiyo
 ya mfanikio pamoja na vikwazo vyote walivyokutana navyo.

Kuna siri imejificha hapa?
Ndio, 
kushindwa mara nyingi na bado kuendelea kunga'ang'ania mpaka unashinda,
 inaonyesha kuna kitu
 alikiona hapo.

Ni kipi hicho?
Nadhani,
 tunahitaji makala itakayojitegemea, 
kuelezea siri iliyopo 
hapa kwa watu wengi
 waliofanikiwa.

Unapopatwa na wakati mgumu,
 iwe katika masomo au kazini 
hupaswi kukata tamaa mapema 
bali 
tumia historia fupi za watu hawa kujitia 
nguvu ya kusonga 
mbele.

Watu hawa waliofanikiwa wapo katika makundi makuu 8.
Leo tunaanza na kundi la kwanza la 
wafanya biashara.

1.Henry Ford:
Huyu ni mfanyabiashara raia wa Marekani,
alizaliwa 
30 julai 1863 katika familia ya wakulima wadogo,
 na kufa 7 Aprili 1947.
Ndiye aliyeanzisha
 kampuni kubwa ya magari aina ya Ford.
 Aliondoka kwao,
 akiwa na miaka 16 tu
 na kwenda kutafuta 
ajira ya umakenika.
Kabla hajafanikiwa,
 alifilisika kibiashara mara tano.
 Alianza kuonja mafanikio baada ya kubuni 
gari la kwanza kutengenezwa 
Marekani aina ya 
Ford Model T.

2.R. H. Macy:

Ni raia wa Marekani
 ambaye alikuja kuanzisha 
biashara ya idara ya stoo kubwa za biashara
 katika jiji la
NewYork.
Alizaliwa 30 Agosti 1822 na 
kufariki 29 machi 1877.
Kabla hajafanikiwa katika wazo hili alifeli mara saba.

3.F.W. Woolworth:
Huyu ni raia wa Marekani ambaye alifanya kazi katika stoo ya bidhaa ya 
mfanyabishara mwengine,
ambako alipokea manyanyaso 
mengi hadi yakamfanya 
aamue kukaa chini na 
kupata wazo la yeye kufungua stoo zake mwenyewe za biashara.
Alizaliwa 13 Aprili 1852 na
kufa 8 Aprili 1919. 
Hata huku Tanzania kuna maduka yenye hili 
jina lake moja 
maeneo ya Posta PPF Tower.

4.Soichiro Honda:
Ni raia wa Japan,
na muanzilishi wa kampuni ya Honda.
Aliwahi mara kadhaa kuomba 
kazi katika kampuni ya
 Toyota kama injinia,
lakini alikosa baada ya 
kufanyiwa usaili na 
kuonekana hana vigezo.
Alikaa muda mrefu sana bila kuwa na 
kazi,
 kitu kilichomfanya 
akae chini kufikiria na kuibuka na 
wazo la 
kampuni ya Honda.
Alizaliwa 17 Novemba 1906 na
 kufa 5 Agosti 1991.
 Ambayo imekuja kuwa mpinzani wa kampuni iliyomkataa.

5.Akio Morita:
Ni raia wa Japan,
na muanzilishi wa
 kampuni ya Sony.
Bidhaa yake ya kwanza,
 kuanzisha ilikuwa ni 
jiko la kupikia mchele(Rice cooker) 
ambayo ilikuwa inaunguza sana wali hivyo watu waliacha kununua bidhaa hiyo.
Lakini,
 hakukata tamaa mpaka 
alipokuja kuboresha na 
kuja kukubalika tena na bidhaa 
nyingi tofauti tofauti
 za vifaa vinavyotumia umeme.
Alizaliwa 26 Januari 1921
na kufa 3 Oktoba 1999.

6.Bill Gates:
Ni raia wa Marekani,
alizaliwa 28 Oktoba 1955 mpaka leo bado anadunda.
Alianza na mkosi wa kufukuzwa
 chuo cha Harvard
ambapo aliamua kuanzisha biashara 
na mwenzake kwa jina la kampuni 
iliyoitwa Traf-O-Data 
ambayo 
haikufanikiwa kabisa.
Alipopata wazo la kutengeneza kompyuta alilipeleka katika kampuni moja ambapo lilikataliwa.
Hakukata tamaa na mwisho wa uvumilivu wote akaja na kampuni ya 
Microsoft ambayo imempa utajiri 
usioelezeka.

7.Harland David Sanders:
Ni raia wa Marekani,
na muanzilishi wa kampuni ya kukaanga kuku ya Kentucky Fried Chicken(KFC).
Alipoanza hii biashara alikataliwa mara 1,009 na migahawa ya Marekani kumpa 
oda ya kuku anaouza.
Lakini uvumilivu wake ukaja kumpa mafanikio makubwa katika biashara hiyo hiyo.
Alizaliwa 9 Septemba 1890 na 
kufa 16 Desemba 1980.

8.Walt Disney:
Kwa wale wapenzi wa 
filamu na katuni,
huyu ndio mtu aliyewaingizia 
hiyo burudani kwa mafanikio sana.
Alianza kwa kufanya kazi ya 
uhariri wa gazeti 
ambapo alifukuzwa kwa 
kuonekana hana ubunifu.
Na alikuja kuanzisha miradi 
 mbali mbali ambayo haikuweza kudumu muda mrefu na kumfilisi kabisa.
Lakini mwisho wa uvumilivu wake akaja kufanikiwa katika 
kampuni yake ya Disney ambayo 
inajihusisha na filamu na katuni.
Alizaliwa 5 Desemba 1901 na 
kufa 15 Desemba 1966.
USIOGOPE KUSHINDWA,
KILA KITU USIPOJARIBU
 HAUTAWEZA KUKIJUA KAMWE.

KAMA WEWE UNATAKA KUFANYA BIASHARA 
AU 
ULISHAANZA,
 UKISHIDWA USIKATE TAMAA.
 ENDELEA KUNG'ANG'ANIA KAMA 
UNAJUA NDICHO KITU PEKEE UNACHOWEZA KUFANYA 
KATIKA MAISHA YAKO.
USIKATISHWE TAMAA NA WAFANYABIASHARA AMBAO WANADHANI WANAFAHAMU KILA KITU ,
KWA KUKOSOA WAZO LAKO.
 NAO PIA KUNA VITU HAWAJUI HATA KAMA WAMESHAFANIKIWA KWA HIYO PIGANIA ULICHONACHO.

Wednesday, 11 September 2013

Usikate Tamaa Kamwe

Kama umeshindwa jambo
 na unafikiria 
kuwa upo mwisho wa safari yako 
na huna sehemu nyingine ya kwenda,
tambua 
unajidanganya nafsi yako.

Umejifunga jela mwenyewe 
na mawazo yako ya 
kujikatisha tamaa.

Kwa kufikiria hivyo 
ni kujitengenezea nafasi ndogo ya kufanikiwa katika unalofanya,
 na nafsi yako itaanza kuamini wewe ni 
mtu wa kushindwa.

Tunaishi katika ulimwengu wenye njia nyingi za kufanikiwa katika 
yale tunayojihusisha nayo.
Haya ndiyo unapaswa uyafikirie kabla ya kukata tamaa:

1.UMERIDHIKA NA KUSHINDWA?

Kushindwa si kuanguka chini;
ila ni kushindwa kunyanyuka wakati una nafasi ya kunyanyuka.
Mara nyingi ni lazima kushindwa mara nyingi ili ufanikiwe.
Na ndio maana unaposhindwa mara moja sio mwisho wa kila kitu.
Wazo lako lolote ambalo limeshindwa 
kufanya kazi,
linafungua njia ya wazo litakaloshinda.
Ukishindwa na ukaanza kukubaliana na 
hilo maana yake ni 
kuridhika na kushindwa.

2.UMEJIFUNZA NINI LA MUHIMU?

Maisha siku zote yanatoa nafasi ya pili,
ili usahihishe makosa.
Lakini
 nafasi hii ya pili haitakuwa na 
maana yoyote kama hakuna ulilojifunza 
katika kosa lililopita.
Unatakiwa ukubali udhaifu wako 
lakini
 kusanya nguvu kupitia hayo na ujifunze kitu ndani yake.
Unapofanya kosa 
chukua nafasi ya kutafuta nafasi ya pili kusahihisha kosa hilo
 na ukusanye uzoefu mpya.

3.WEWE NDIO WA KWANZA KUKUTANA NA MAGUMU?

Maisha huanza na maisha huisha,
kuna muda maisha yanacheka na maisha yanalia,
maisha yanakata tamaa na 
maisha yanajaribu.
Maisha yana picha tofauti katika macho ya kila binadamu aliye juu ya ardhi.
Ukweli ni kuwa vile ulivyokuwa zamani,
ulivyo sasa na 
yule utakayekuja kuwa ni 
watu watatu tofauti.

4.MAUMIVU YAMEKUSAIDIA NINI?

Kuna muda lazima mambo yabadilike ili na
 wewe ubadilike.
Lazima kuna muda upate maumivu ili ukue kiuzoefu.
Kuumia ni lazima ili upate hekima ambayo haukuwahi kuiwaza kama utaipata.
Lazima uumie moyo 
ili uanze kuufuata moyo wako katika 
maamuzi sahihi.

5.KUFANIKIWA NI KUWA NA NINI?

Usiruhusu mahangaiko yako ndio yakutambulishe kwa watu wewe ni nani.
Sio kila kitu unavyokitarajia kiwe kitakuwa hivyo hivyo ulivyodhani wewe.
Na ndio maana unapaswa kuacha kuishi matarajio,
ishi wakati ulionao na fuata mkondo na si kwenda kinyume na njia ya mkondo.
Jikumbushe kuwa ni ukamilifu kutokuwa mkamilifu.
Mafanikio si kitu unachopata,
ila ni uwezo wako wa kufanyia kazi uliyojifunza na kuyatumia kwa ufanisi katika uhalisia wa maisha yako.

6.KUNA NJIA NYINGINE YOYOTE?

Tofauti ya njia nyembamba na ndogo inajengwa na mtazamo wako.
Na hapo ndio unapaswa ujue kuwa ili kubadilisha kitu ni lazima ubadilishe 
mtazamo wako.
Kutoweza kuona njia mbadala 
katika maisha yako inatokana na
 mtazamo wako 
kujifungia eneo moja la maisha.

7.KUNA JAMBO LINAWEZA KUFANIKIWA BILA KIKWAZO?

Hata kama haupo
 sehemu ambayo ulitamani kuwa haimaanishi kuwa hautakuwa siku moja.
Kufanikiwa kunaambatana na kujitambua ambapo kutakusaidia kupambana 
mpaka mwisho.
Mafanikio bila ya vikwazo vitakufanya usione thamani yake
 na unaweza kuyatumia vibaya.
Ukuta uliokutenga na ndoto yako unakusaidia kufahamu ni jinsi gani utajitoa kufikia unalotamani kwa kuuvunja.

8.ZURI NI HILO TU?

Unaweza ukawa umekutana na mabaya wakati unatafuta mazuri fulani,
lakini
haimaanishi hayo mazuri uliyoyakosa ndio pekee yaliyopo duniani.
Maisha yana mambo mengi mazuri na 
si yale tunayodhani sisi 
kuwa ni mazuri na kuyaona mengine kuwa mabaya kwa kuwa ndivyo tunavyodhani.

KUKATA TAMAA KATIKA MAISHA, 
SI KITU 
CHA KUKIFIKIRIA KWANZA PALE UNAPOKUMBANA 
NA MAGUMU.

HAKUNA UTAKALOPANGA KULIPATA,
 UKALIPATA KIRAHISI RAHISI KAMA WENGI WETU TUNAVYOTAMANI IWE.

TUMIA MASWALI HAYO HAPO JUU,
 KUJIULIZA PALE UNAPOKUMBANA 
NA WAKATI MGUMU ILI USIKATE TAMAA