Fanikiwa kimaisha kwa kuyaweka haya katika matendo !!
Ili
uweze kufanikiwa maishani unatakiwa uwe na mipango ya maisha yako.Mara
nyingi watu wengi wamekuwa ni hodari wa kupanga mipango ya harusi na
mambo mengine madogo madogo lakini wanasahu kupanga mipango ya maisha
yao. Kama huna mipango juu ya maisha yako si rahisi kupata mafanikio.
Kuweka malengo ni mchakato wa kufikiria juu ya maisha yako ya baadaye na
kuyabadili kutoka kwenye hali duni au hali uliyonayo kwa sasa na kuwa
yenye mafanikio. Maisha ni safari ndefu hivyo ni vyema ukajua unakwenda
wapi na utafikaje huko unapotaka kwenda.Kujua malengo yako kutakusaidia
kuwa na muelekeo na kukusanya nguvu zako zote kwenye jambo unalolitaka.
Mara nyingi huwa nawauliza watu swali hili ninapiojadili kuhusu malengo,
Jee kama unasafiri na hujui unakokwenda ukifika kwenye kituo cha magari
ya kubeba abiria utapanda gari la kwenda wapi? Wengi hunijibu kwamba
utapanda gari lolote na kwa sababu hiyo, kwa vile hujui unakokwenda kwa
hakika huwezi kufika huko. Huo ndiyo umuhimu wa kuweka malengo kwani ni
sawa na msafiri anayejua anakokwenda hivyo akifika kituoni atajua apande
gari gani na hakika atafika anakokwenda. Kwa hiyo si swala la ajabu
kuona watu wengi wakihangaika kutafuta mafanikio bila kuchoka lakini
hawafanikiwi kwa sababu ya kutojua siri hii.
Kutokuwa na
malengo kumewafanya watu kufanya shughuli nyingi kwa wakati mmoja na
vilevile kuziacha baada ya kuona kwamba ni ngumu.Watu hawa hufanya hivyo
kwa kushawishiwa au kwa kuiga baada ya kuona wengine wakifanya biashara
ya aina fulani. Ndiyo maana mtu mmoja akianzisha duka mtaani basi watu
wengine nao wanaanzisha duka na hivyo unakuta maduka mengi katika mtaa
huo mpaka mengine yanakosa wateja.Mimi mwenyewe nimewahi kukumbwa na
tatizo hili, nimefanya biashara nyingi sana, nimewahi kufanya biashara
ya mtandao kuuza bidhaa za makampuni kadhaa, ukandarasi, vyuma chakavu
na kutengeneza chaki. Baada ya kutafuta ushauri nilifundishwa namna ya
kujiwekea malengo ndipo nikaamua kutoa huduma ya ushauri wa biashara.
Kwa sasa hivi kwa vile ninajua ninachokitaka na nimekwisha jiwekea
malengo yangu siwezi kuyumbishwa na kujishughulisha na biashara
nyingine.
Upangaji wa mipango na kuweka malengo hufanywa na
Wafanyabiashara wakubwa, wanamichezo maarufu na wasanii maarufu.
Utaratibu huu huwasaidia kuwapa muelekeo na malengo ya muda mfupi yaani
mwaka mmoja, muda wa kati yaani miaka mitatu hadi mitano na na muda
mrefu yaani miaka kumi na kuendelea. Pia huwasaidia kukusanya nguvu na
maarifa ili kufikia malengo yao kwa urahisi. Malengo huanzia kwa kuwa na
picha kubwa ya hali halisi unayoitaka kwa kujiuliza ni nini
unachokitaka maishani mwako? Na kisha huvunjwa vunjwa kidogo kidogo .
Maisha ya binadamu yamegawanyika klatika sehemu mbali mbali kama vile
kiuchumi kiafya kisaikolojia na kiafya. Kwa mfano,mafanikio ya ya
mwanafunzi hupimwa kwa maksi zake anazopata darasani lakini kiuchumi ni
jinsi alivyo na pesa nyingi benki pamoja na vitegauchumi alivyonavyo
pamoja na shughuli anayoifanya ambayo inamuingizia kipato. Mambo mengine
ni mahusiano mazuri aliyonayo kwenye jamii na familia yake. Pia bila
kusahau afya yake, kwani hakuna utajiri mkubwa kwa binadamu kuliko afya
yake.
Mambo muhimu ya kujiuliza katika kupanga malengo ni yafuatayo;
Jee unataka kufanya kazi au shughuli gani maishani mwako? Jee
ungependa kupata fedha kiasi gani kutokana na shuguli unayotaka
kuifanya? Jee maarifa/elimu ipi ambayo ungependa kuipata ili kuweza
kukusaidia kufikia malengo yako? Mtazamo gani au ni mabadiliko yapi ya
tabia unayotakiwa kuyafanya ili ufikie malengo yako? Tafakari mambo haya
. Wataalamu wa maswala ya biashara wanashauri ufanye biashara ambayo
inaendana na kipaji au elimu yako, kwani kwa kufanya hivyo utapunguza
muda wa kujifunza mambo mapya. Mara nyingi kuamua ufanye biashara gani
ni suala gumu na mimi nimekuwa nikikutana na watu wakiwa na mtaji lakini
hawajui wafanye biashara gani.
Baada ya kupanga mipango yako
kama nilivyokueleza hapo juu unatakiwa kuanza utekelezaji mara moja. Ni
vyema kila mwaka unapoanza uwe na mipango pamoja na malengo ya mwaka huo
na inapofika mwisho wa mwaka unaangalia malengo yapi uliyoyatekeleza na
yapi hukuyatekeleza. Pia ujiulize sababu zilizosababisha usitekeleze
malengo hayo. Yale mambo/ malengo ambayo hukuyatekeleza mwaka uliopita
unapaswa kuyatekeleza mwaka unaofuata. Katika utekelezaji si mambo yote
unaweza kuyafanya kwa mara moja unaweza kuyapangia mipango kwa mfano
kila siku unaweza kuorodhesha mambo utakayofanya kesho yake kuanzia saa
12 asubuhi saa mpaka saa 12 jioni jambo linaloshindikana leo unalipeleka
kesho. Vivyo hivyo unaweza kupanga mambo utakayoyatekeleza ndani ya
wiki moja na ndani ya mwezi mmoja.
Mwongozo wa namna ya kuweka malengo;
Malengo yaelezewe kwa njia chanya mfano tumia neno ninataka kuwa tajiri
badala ya kuwa ninataka kupambana na umasikini. Unatakiwa kutaja ni
kiasi gani cha pesa uunachokitaka na pamoja na muda gani/lini unataka
upate pesa hizo. Unakiwa uweke vipaumbele kutokana na uzito wa malengo
yako ili ujue unaanza na jambo lipi na kumalizia na jambo lipi. Malengo
yako lazima yaandikwe na ili yasuisahaulike pia unapaswa kuyasoma mara
kwa mara ili usiyasahau. Njia nyingine ya kukusaidia kukukumbusha kuhusu
malengo yako ni kwa kutumia picha. Unaweza kukata picha ya kitu
unachokitaka kwenye magazeti, kwa mfano kama unataka kununua gari ya
aina fulani unaweza kukata picha hiyo na kuibandika sehemu ambayo
unaiona kila mara kama vile kwenye kabati mlango wa chumbani au kwenye
kabati. Unaweza kumweleza mtu unayemwamini kuhusu malengo yako mfano
mkeo mwanao mkubwa au rafiki wa karibu ili aweze kukuhoji kama hutaweza
kufikia malengo hayo. Malengo yako usimwambie kila mtu kwani watu
wengine wanaweza kukufitini na kukukwamisha. Weka malengo ambayo
yanawezekana au yanatekelezeka kufuatana na uwezo wako,kwa mfano usiweke
malengo ambayo yako nje ya uwezo au mazingira yako kama vile katika
biashara, kupanga mipango ambayo haiendani na sheria za nchi mfano
kufanya biashara bila leseni.
Katika kufikia malengo yako
furahia hali kama malengo uliyoyapanga yalikuwa magumu basi jipongeze.
Kama yalikuwa mepesi basi jipangie magumu zaidi. Kama yalikuwa magumu
sana yapunguzie makali. Kushindwa kufikia malengo si tatizo jizoeze
kufanya utaratibu huu kwani unaweza kukusaidia kukufikisha mbali
kimaisha. Ukishindwa kufikia malengo kipindi hiki jaribu kuyapeleka
mbele mwaka ujao. Katika maisha usikate tamaa kwani ukikata tamaa ni
sawa na kuwa mfu. Watu mashuhuri wamethibitisha kwamba unaposhindwa
kufikia malengo hiyo ni kama shule ya maisha jaribu tena na tena mwisho
utafanikiwa.
Jee umekwisha jiwekea malengo katika maisha yako?
Kama hujafanya hivyo nakushauri uanze sasa hivi na utaona jinsi
utakavyoanza kuyapata mafanikio kwa haraka
No comments:
Post a Comment